USHEMASI 2024, 25 Januari
Tarehe 25 mwezi wa kwanza katika sikukuu ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo kuliadhimishwa jimboni kigoma katika seminari ya Mt. Yosefu Iterambogo misa takatifu na kutoa daraja ya ushemasi kwa mafrateli; Flavian Joseph Lutakangwa na Petro Leonard Kabage, kwa kuwekwa Wakfu na Mhashamu Askofu Joseph Mlola ALCP/OSS Askofu wa Jimbo la Kigoma.
katika homilia yake baba askofu, alikazia juu ya umuhimu wa kuongoka kwa wakristo na kumrudia Mungu hasa kuishika na kuilinda imani katika wakati huu wenye mtikisiko sana wa imani kutokana na wimbi la imani potofu ya ramli chonganishi maarufu kama Kamchape. alitumia nafasi hiyo kuwatahadharisha na kuwaeleza mashemasi mazingira ya wanakokwenda kuhudimia na waamini watakao wahudumia waaishio katika sekeseke hili la imani ya kichawi maarufu kama Kamchape.
pamoja na hayo, mhashamu baba askofu aliwaeleza juu ya majukukumu yao msingi kama mashemasi; “Wakisha imarishwa kwa kipaji cha Roho Mtakatifu watakuwa wasaidizi wa Askofu na Mapadri wake katika huduma ya Neno, ya altare na ya upendo, nao wakijifanya watumishi wa wote. Kama wahudumu wa altare wataihubiri Injili, wataiandaa sadaka na kuwagawia waamini Mwili na Damu ya Kristo.Aidha, kama watakavyoamriwa na Askofu, itawapasa kuwashauri na kuwafundisha mafundisho matakatifu waamini na wasio waamini, kuongoza sala, kutoa Ubatizo, kusimamia na kubariki ndoa, kuwapelekea waliopo kufani Komunyopamba, kuongoza ibada ya mazishi.”
HISTORIA FUPI YA SHEMASI FLAVIAN JOSEPH LUTAKANGWA
Shemasi Flavian Joseph Lutakangwa alizaliwa mnamo tarehe 24-05-1993, saa 9:00 katika kijiji Mvugwe, amekulia na kulelewa katika Kijiji cha Nyamidaho. Flavian ni mtoto wa kwanza kuzaliwa katika Familia yenye Watoto jumla nane (8) kwa Baba Joseph Lutakangwa na Mama Anatoria Yilagera Nkushi.
ELIMU
Alianza darasa la awali mwaka 2001 na Shule ya Msingi mwaka 2002 hadi 2008 katika Shule ya Msingi Nyamidaho.Alijiunga na masomo ya awali ya kidato cha kwanza (Pre- form One) mwaka 2008 kwa muda wa miezi mitatu (3) katika Shule ya Sekondari ya Mtakatifu Mathias Mulumba- Janda. Na baadae Kidato cha Kwanza hadi cha nne mwaka 2009 hadi 2012 katika Shule ya Sekondari Mwilamvya iliyopo Kasulu.Mwaka 2013 hadi 2015 alijiunga na Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Ihungo (Ihungo Boys Secondary School) kwa mchepuo wa Sayansi (Physics, Chemistry na Biology (PCB)).
SAFARI YA KIROHO NA WITO
Shemasi Flavian anasema; “Ambacho ninakikumbuka mpaka sasa ni kwamba kwa mara ya kwanza niliwahi kuwatamkia nyumbani ya kuwa nitakuwa Padre nikiwa chekechea hapo nilikuwa nina umri wapata miaka saba (7). Basi nikiwa darasa la Tano (2006) yaani mwaka mmoja mbele baada ya kuanza mafundisho ya Ukatekumeni niliandika barua ya kujiunga na Seminari ndogo ya Iterambogo licha ya kwamba nilikuwa bado sijabatizwa. Lakini nilidumu katika bidii ya Sala na kumwomba daima Mungu kwamba siku moja anifanye kuwa chombo chake cha kuihubiri Injili kwa watu wote. Nilibahatika kufanya mtihani huo baada ya kumaliza darasa la saba. Kwa bahati mbaya sikuchaguliwa, lakini nikasema Mungu anampango nami. Hatimaye kiu yangu ilitulia baada ya Kubatizwa mnamo tarehe 13-07-2008, ikiwa ni pamoja na Ekaristi Takatifu pia Kipaimara katika Kanisa la Parokia ya Mt. Luka-Makere na Paroko Padre Vedastus Nyamrundwa. Nilibatizwa Jina FLAVIAN na Msimamizi wangu wa Ubatizo ni Lameck Method aliyekuwa Katekesta. Niliendelea kulipenda Kanisa na watu wake, nikiwa kama mwana TYCS katika shule nilizopita na kuwa kiongozi kwa nafasi mbalimbali”.
MALEZI YA KIPADRE
Mnamo tarehe 01-06-2015 Shemasi Flavian aliomba kujiunga na Nyumba ya Malezi ya Watakatifu Petro na Paulo Mitume –Iterambogo. Baadae alichaguliwa kujiunga na Malezi kwa Masomo ya Falsafa katika Seminari Kuu ya Mama Bikira Maria Malkia wa Malaika-Kibosho, Moshi mwaka 2015 hadi 2018.
Baada ya Masomo ya Falsafa, alichaguliwa na kujiunga na Masomo ya Teolojia katika seminari kuu ya Kipalapala – Tabora kuanzia mwaka 2018 hadi 2022 (Miaka 4).
UTUME
Shemasi Flavian, ameweza kupangwa Parokia mbalimbali za Jimbo letu la Kigoma kwa Uchungaji mdogo kama ifuatavyo:Parokia ya Mt. Klara Kidahwe (wakati yuko Nyumba ya Malezi).
- Mwaka 2016, alipangwa Parokia ya Mt. Maria -Kibondo.
- Mwaka 2017, alipangwa Parokia ya Mt. Teresia wa Mtoto Yesu- Muhange.
- Mwaka 2018, alipangwa Parokia ya Mt. Karoli- Lwanga- Kalinzi.
- Mwaka 2019, alipangwa Parokia ya Mt. Yosefu Mfanyakazi- Kiganza.
- Mwaka 2020, alipangwa Parokia ya Mt. Karoli- Lwanga- Kalinzi.
- Mwaka 2021, alipangwa Parokia ya Mt. Remigius -Kagunga.
- Uchungaji mkubwa Mwaka 2022-2023 katika Parokia ya Mt. Yohane XXIII -Kumsenga. Pia Uchungaji mkubwa katika Seminari ndogo ya Mtakatifu Yosefu Iterambogo (Mwalimu na Mlezi).
HISTORIA FUPI YA SHEMASI PETRO LEONARD KABAGE
Shemasi Petro alizaliwa mnamo tarehe 23-08-1993, katika kijiji au Kigango cha Nyarubanda, Parokia ya Bikira Maria Mlango wa mbingu Muhinda. Wazazi wake ni Leonard Petro Kabage na Adelaida Nkwila Gwoma.
ELIMU
Shemasi Petro Leonard alianza darasa la kwanza rasmi mwaka 2002 hadi 2008 alipohitimu Elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Nyarubanda. Alijiunga na masomo ya Kidato cha Kwanza hadi cha nne kuanzia mwaka 2009 hadi 2012 katika Shule ya Sekondari Nyarubanda.
Kisha mwaka 2013 hadi 2015 alichaguliwa na kujiunga na Shule ya Sekondari ya Kalangalala(Geita) kwa mchepuo wa Sayansi (Physics, Chemistry na Biology (PCB). Baada ya masomo hayo ya sekondari alikata shauri ya kuendelea kuiitikia sauti ya mungu kwa kujiunga na nyumba ya malezi ya upadre ya watakatifu Petro na Paulo Iteramabogo mwezi octoba mwaka 2015. Katika kipindi cha malezi 2015/2016 alipata elimu ya Ushauri wa Kichungaji (Clinical Pastoral Education) Bugando Mwanza.
Alijiunga na masomo ya falsafa kama frateli katika seminari ya mtakatifu Antoni wa Padua Ntungamo-Bukoba kwa kipindi cha mwaka 2016-2019. Baada ya masomo hayo aliendelea na malezi na masomo ya TaaliMungu (Teolojia) Katika seminari kuu ya Mtakatifu Paulo Kipalapala kati ya mwaka 2019-2023.
UTUME ( UCHUNGAJI )
Shemasi Petro alipata kuhudumu/Kufanya utume katika parokia mbalimbali jimboni ambazo ni Parokia ya Mt. Terezia wa Avila-Nyaronga, Parokia ya Mt. Pankrasi-Kasanda, Parokia ya Mt. Klara-Kidahwe, Parokia ya Mt. Maria Malkia wa Amani-Kasumo,Parokia ya Mt. Maria Mama wa Mungu-Kibondo na Chuo cha Katekesi-Kasulu.
Uchungaji mkubwa katika Parokia ya Mtakatifu Remigius Kagunga
SAFARI YA KIROHO NA WITO
Hemasi Petro anasema, “nilitamani kuwa Padre tangu nikiwa mdogo, nilivutiwa sana na maisha ya kipadre na nikatamani kumtumikia Mungu na watu kama Padre. Nilipokua nasoma sekondari niliteuliwa kuwa msaalishaji katika vipindi vya dini vya TYCS. Nilitumika katika chama cha TYCS kama msalishaji lakini pia kama mwalimu wa kwaya. Hii (majukumu hayo) ilizidi kuniimarisha katika nia yangu ya kutaka kumtumikia Mungu na watu wake wote. Zaidi ya hayo, watu mbalimbali walizidi kunitia moyo katika nia hiyo”.
Related Posts
BAHASHA YA JIMBO
On 7th December 2023, the diocese of Kigoma held an event known as “BAHASHA YARead More
SHEREHE YA UWUKI
Pongezi kwa Wajubileani wa miaka 25 katika utume, Upadre na Utawa. Tarehe 19 Octoba 2023,Read More
PRIEST’S ANNUAL RETREAT 2023
from October 2 to October 6, priests who work in the Diocese had a momentRead More
Comments are Closed